WALIOMTUKANA SPIKA SASA KUSAKWA
POLISI mkoani Dar es Salaam wametangaza kuwafuatilia,
kuwasaka na kuwachukulia hatua wote waliotuma ujumbe wa matusi ama
kupiga simu ya vitisho kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Viongozi wa Chadema walifanya mkutano wao mwishoni mwa wiki kwenye
Viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke, jijini Dar es Salaam na kutoa namba za
Spika wa Bunge ili mashabiki wamshinikize ajiuzulu.
Pia viongozi hao walitoa namba za simu za Naibu Spika, Job Ndugai ili
naye ashinikizwe ang’oke katika nafasi yake kwa madai ya kukandamiza
upinzani bungeni.
Chadema walidai kuwa Makinda na Ndugai wamekuwa wakipindisha kanuni
wakati wa kuliongoza Bunge. Pia walidai kuandaa taarifa ya kutokuwa na
imani na maspika hao, ripoti ambayo wataiwasilisha kwenye Bunge lijalo.
Wakati Polisi wakitangaza hayo, juzi Ofisi ya Bunge kupitia kwa
katibu wake, Thomas Kashilillah ilisema itawachukulia hatua kali wale
wote waliotumia lugha chafu kwa ujumbe mfupi ama kupiga moja kwa moja
kwa Spika na Naibu wake.
Hatua hiyo ya polisi inachukuliwa baada ya Makinda kudai kuwa
ametumiwa ujumbe mfupi zaidi ya 400 na kupigiwa simu zisizopungua 200,
zinazomkashifu na nyingine zikiwa ni za vitisho dhidi yake.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi
alisema Polisi watafanya uchunguzi kuwabaini wote waliohusika kufanya
hivyo na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ili iwe fundisho
kwa wengine. Msangi alisema kuwa taarifa hizo wamezipata jana na
walijipanga kuhakikisha wahusika wote wanatiwa mbaroni.
“Polisi tumeanza kuwafuatilia waliomtukana Spika na lazima tuwakamate kwani kitendo hiki ni kinyume cha sheria,” alisema Msangi.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Kaimu Ofisa Mawasiliano
wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala alisema
suala la vitisho kwa mtu yeyoye linahusu hasa Jeshi la Polisi na kwamba
wao ndio wanaopaswa kuchukua hatua zaidi za kisheria.
Wanachama wa CCM Mkoa wa Iringa, wamelaani vikali kitendo cha baadhi
ya wafuasi wa Chadema kutuma ujumbe mfupi wa simu za mkononi kumkashifu
Makinda huku baadhi yao wakipendekeza chama hicho kifutwe kwa kukosa
ustaarabu.
Katibu wa Baraza la Wazee wa CCM Wilaya ya Iringa, Said Mdota alisema
kitendo alichofanyiwa Spika Makinda si cha kiungwana na hakikubaliki na
wapenda amani wote. Mdota alipendekeza wahusika wote wasakwe na
wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya wa Wanawake Mkoa wa Iringa, UWT, Zainab
Mwamwindi alisema jumuiya hiyo inatarajia kukutana kesho pamoja na
agenda nyingine itajadili suala hilo na kulitolea tamko.
“Sisi kama wanawake na Spika ni mwanamke, suala hili limetudhalilisha
sana na katika hili tunalikemea kwa nguvu zote na Februari 14,
tunatarajia kufanya kikao cha Kamati ya Utendaji tutalijadili na
kulitolea tamko,” alisema.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment