Home »
Matukio
» SAKATA LA MSICHANA KUCHINJWA NA MPENZI WAKE
SAKATA LA MSICHANA KUCHINJWA NA MPENZI WAKE
VILIO vilitawala Kata ya Nyahanga wilayani hapa wakati wa kuuaga
mwili wa binti Jessica Elialinga (19) aliyeuawa kinyama kwa kuchinjwa
kama kuku na mpenzi wake, Musa Petro (27) mkazi wa Shunu kwa sababu
zinazodaiwa ni wivu wa kimapenzi.
Jessica Elialinga baada ya kuchinjwa.
Tukio hilo lililoibua simanzi kubwa kutokana na marehemu kuhitimu
Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Nyihogo, Kahama
mwaka jana, lilijiri saa 12:45 Februari 6, mwaka huu.Kitendo hicho
kilifanyika katika banda la mbuzi lililopo nyumbani kwa kijana huyo
ambaye baada ya kutekeleza mauaji na yeye alifanya jaribio la kutaka
kujitoa roho kwa kisu.Akisimulia juu ya tukio hilo, rafiki wa
karibu wa Musa ambaye aliomba hifadhi ya jina lake kwa ajili ya usalama,
alisema wiki moja kabla ya tukio hilo, mtuhumiwa huyo alikuwa
akiwatangazia jamaa zake kwamba ana dhamira ya kumuua binti huyo
kufuatia kubaini kuwa anamsaliti kimapenzi.
Muuaji Musa Petro.
“Unajua Musa anafanya kazi ya kuchuna ngozi za wanyama machinjio ya
Wilaya ya Kahama, alitutangazia dhamira yake hiyo, lakini tulichukulia
kauli yake kama mzaha.
“Alisema anataka kufanya hivyo kwa sababu
amekuwa akitumia gharama kubwa kwa mpenzi wake huyo tangu walipoanza
uhusiano, msichana akiwa kidato cha pili, lakini anatoka kimapenzi na
mwanaume mwingine,” alisema rafiki huyo.
Hata hivyo, inadaiwa baada
ya mtafaruku wa usaliti, wawili hao walipatana na kuendelea na mapenzi,
lakini baada ya mwanafunzi huyo kuhitimu kidato cha nne alibadilika
ambapo mwanaume alisikia kuwa tayari ana mwanaume mwingine kutoka jijini
Mwanza ambaye walikubaliana kufunga pingu za maisha baada ya kumaliza
masomo
Jessica Elialinga enzi za uhai wake.
Inadaiwa siku chache kabla ya mauaji hayo, rafiki mmoja wa karibu wa
mtuhumiwa alikutana na marehemu njiani na kumsimamisha kwa lengo la
kumweleza kauli zenye kutishia maisha yake anazozitoa mpenzi wake,
lakini binti huyo hakusimama kumsikiliza.
Baada ya Musa kudaiwa
kufanikiwa kumchinja mpenzi wake huyo na yeye kujikata koromeo na kuanguka
akiwa ameishiwa nguvu, kijana mchunga mbuzi ambaye wengi katika eneo
hilo humchukulia kama kaka yake Jessica, ndiye aliyekuwa wa kwanza
kumshuhudia Musa akiwa katika hali hiyo.
Alipomhoji kulikoni,
hakupata jibu zaidi ya kushuhudia jitihada za mtuhumiwa huyo kufungua
mlango wa chumbani mwake zikishindikana.
Kijana huyo alitoa taarifa kwa watu ambao walifika na kumchukua Musa na kumkimbiza hospitali ya wilaya kuokoa uhai wake.
Watu waliobaki nyumbani walifuatilia michirizi ya damu hadi kwenye zizi
la mbuzi ambako walimkuta Jessica ameshafariki dunia baada ya
kuchinjwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi wa
Polisi, Everest Mangala alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo
alisema mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani Kahama katika
Hospitali ya wilaya hiyo anakoendelea kupatiwa matibabu.
0 comments:
Post a Comment