WATU wawili wamefariki dunia na wengine 36 wamejeruhiwa vibaya baada ya basi la kampuni ya Bunda Express walilokuwa wakisafiria, kuacha njia na kupinduka katika kijiji cha Ngashe kata ya Kahangara wilayani Magu mkoani Mwanza.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ernest Mangu ajali hiyo ilitokea jana saa 2 asubuhi katika barabara kuu ya Musoma- Mwanza na kuhusisha basi lenye usajili namba T 782 BKZ lililokuwa likitokea wilayani Bunda kwenda Mtukula mpakani mwa Tanzania na Uganda.
Alimtaja marehemu kuwa ni Kiyumba Kasarara (80) mkazi wa Kibaoni Muleba, mkoani Kagera na mwingine jina lake halijatambulika.
Alisema majeruhi 22 wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Magu huku wengine 14 wakikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.
Kamanda Mangu alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa gari hilo ambaye hakuzingatia hali ya hewa ya mvua iliyokuwa ikinyesha kwa wakati huo.
Akizungumza katika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jacqueline Liana alisema ni ajali mbaya iliyotokea wakati huu tunapouanza mwaka mpya na inasikitisha sana.
“Tumejitahidi katika kuokoa majeruhi wengine wameumia kichwani na sehemu mbalimbali mwilini kutokana na kubanwa na viti na kulazimika wengine kuwakimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Magu na wengine Bugando,” alisema.
Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Mwanza, Nuru Selemani akizungumza katika eneo la tukio aliwataka madereva kuwa makini na kuchukua tahadhari wanapokuwa barabarani.