Wakizungumza na Tanzania Daima nyakati tofauti sokoni Kariakoo jana, walisema bei zimekuwa juu kuliko kawaida huku wakitaja vitu kama nguo za shule, mabegi na viatu kuwa ndio vinaongoza.
“Vitu viko juu kweli, kama mimi nina watoto wawili hapa nakuna kichwa, nguo ziko juu, viatu ndo usiseme,” alisema mkazi mmoja aliyefahamika kwa jina la Mama Anna.
Naye, Mariam Said alisema kipindi hiki kimekuwa kigumu kwa wazazi, kwani wanahitajika kununua vifaa vya shule pamoja na kulipa ada wakati maisha yanazidi kupanda juu.
Kwa upande wao, wafanyabiashara walisema hilo si ongezeko la bei bali wanauza kulingana na wanavyonunua vitu hivyo huku wakishindwa kuwaelewa wateja wao kwa kulalamikia bei.