24Bongo News :
Home » , » MAUAJI TENA ZANZIBAR

MAUAJI TENA ZANZIBAR

   MATUKIO yenye taswira ya udini yameendelea kujirudia visiwani Zanzibar ambapo watu wasiofahamika, wamemuua kwa kumpiga risasi Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili, Evarist Mushi, jana asubuhi wakati akiegesha gari lake kanisani hapo.

Hili ni tukio la tatu kutokea visiwani humo ndani ya muda mfupi kwa viongozi wa dini kushambuliwa na kuumizwa, kwani Novemba 5 mwaka jana, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga alimwagiwa tindikali na mtu asiyefahamika iliyomwathiri sehemu kubwa ya mwili wake.

Desemba 26 mwaka jana, watu wasiojulikana walimpiga risasi Padri Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mpendae mjini Zanzibar na kumjeruhi.

Waumini wa kanisa hilo walioshuhudia tukio, walisema kuwa kabla ya Padri Mushi kufika eneo la kanisa, walionekana watu wawili ambao walikuwa na pikipiki wakiwa wamesimama kando ya barabara.

Kwamba alipoingia padri huyo eneo la kanisa kwa ajili ya kuongoza ibada, watu hao walimfuata na kumshambulia wakati akiegesha gari lake, na kisha kukimbia kusikojulikana.

Waumini hao ambao walikusanyika katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, ulipohifadhiwa mwili wa marehemu, waliiomba serikali ichukue hatua kwa wahalifu hao, wakidai matukio hayo yamekuwa yakiwalenga Wakristo.

Akithibitisha tukio hilo, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa alisema kuwa wanaendelea kuwasaka watuhumiwa hao kuwaomba wananchi kutoa msaada wa taarifa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdallah Mwinyi aliiomba serikali kuchukua hatua kwani wahalifu hao wanataka kuleta mfarakano kati ya Wakristo na Waislamu. 

Kanisa laanda tamko 
Askofu wa Jimbo la Zanzibar, Augustino Shayo alifika hospitalini hapo na kujadiliana na baadhi ya viongozi, na baadae mmoja wa viongozi waliokuwa na waumini hao kuwatangazia kurudi kanisani kuendelea na ibada.
Hata hivyo, waumini hao walipinga jambo hilo na kusema kuwa wataendelea kuwapo hapo hadi haki yao ipatikane, huku wengine wakitaka kuandamana ili kuonesha machungu yao.

“Leo tunaandamana tumechoka, tukio la kwanza tumevumilia na hili pia, hapa haki yetu ipo wapi? Tunamtaka Waziri wa Ulinzi kutoa tamko tukiwa hapa hapa," alisema mmoja wa waumini hao.

Kiongozi huyo alirudia tena kuwasihi waumini hao kuwa na moyo wa uvumilivu kama mafundisho ya dini na imani, na kuwaomba waelekee nyumba ya ibada kuendelea na misa ama kurudi majumbani, lakini hawakutii agizo hilo.
 Akitoa msimamo wa kanisa majira ya saa nane mchana, msaidizi wa askofu, Padri John Mfoi aliwataka waumini kurudi nyumbani, na kwamba viongozi wakuu watatoa tamko rasmi hapo baadaye.
"Tayari uchunguzi umeshafanyika na kilichobaki sasa wanamshona na tunasubiri kuoshwa na kisha kuhifadhiwa rasmi. Viongozi wetu wanatarajia kukutana mapema jioni kupanga taratibu zote husika,” aliongeza Padri Mfoi. 
Polisi wajipanga.
Kufuatia mauaji hayo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, alisema kuwa wanawashikilia watu watatu kuhusiana na tukio hilo.
 Akizungumza na waandishi Dar es Salaam jana, Mwema alisema kuwa mara baada ya kupokea taarifa hizo tayari timu ya watu watatu imeenda kwa ajili ya kuanza kazi za kiuchunguzi.
“Taarifa hizo ni za kusikitisha sana na tayari nimetuma timu ya wataalamu waliobobea kwenye masuala ya upelelezi kwenda kufuatilia suala hilo, na tutawakamata tu kwa kuwa tunaweza kupambana na majambazi hatuwezi kuwashindwa wahalifu,” alisema.
Aliitaja timu ya upelelezi iliyokwenda Zanzibar kuwa ni Naibu Kamishna Samson Kasala ambaye atakuwa mpelelezi, Naibu Kamishna Peter Kivuyo kwa ajili ya ukusanyaji taarifa mbalimbali na Simon Siro kwa ajili ya operesheni.
Mwema alizitaja namba za mawasiliano kwa ajili ya kufanikisha upelelezi huo kuwa ni 0754 785557 na 0782 417247, na pia alishauri kutumika kwa namba za makamanda wa polisi wa mikoa, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo kupitia namba hizo.
Alipoulizwa kama mauaji hayo yanahusiana na mtandao wa kundi la Al-Qaeda, Mwema alisema kuwa wamekuwa wakilifuatilia ili kujua lipo kundi hilo.
 Kuhusu lawama za jeshi hilo kuchelewa kuchukua hatua nzito kama hii ya kuunda kundi la wapelezi walivyofanya sasa, alisema kuwa wamefanya hivyo mara kadhaa isipokuwa taarifa hazitolewi kwa uwazi kwa waandishi.Alipoulizwa kama suala hilo linahusiana na masuala ya dini au siasa, Mwema alidai kuwa kuna mwelekeo huo. 

Mbowe aivaa serikali 
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimelaani matukio ya vurugu na mauaji yenye misingi ya tofauti za kidini, huku kikidai ni matunda ya mbegu ya udini na ukabila uliopandikizwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nia ya kuvidhoofisha vyama vya upinzani.
Akifungua kikao cha viongozi wa chama hicho Kanda ya Kaskazini jijini Arusha jana, Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe aliitaka CCM na serikali yake kuhakikisha nchi inakuwa salama.
Alisema CCM kwa kudhani inavikomesha vyama vya upinzani, iliasisi, kueneza na kushabikia sera na chochoko za ubaguzi wa kidini kwa kuwadanganya wananchi kuwa, baadhi ya vyama ni vya kidini na kikabila, matokeo yake sasa udini umeanza kuwa kansa inayoitafuna taifa.
“CCM walidhani chokochoko za udini na ukabila zitaviangamiza vyama vya upinzani na kukisaidia kuendelea kusalia madarakani. Hawakujua wanapandikiza mbegu mbaya miongoni mwa Watanzania waliozoea kuishi kwa amani na umoja bila kujali tofauti zao za kidini na kikabila,” alisema.
Mbowe alisema kuwa CCM wamelikoroga, sasa lazima walinywe kwa kuhakikisha taifa linakuwa moja na lenye amani.
Alisema siyo sahihi viongozi wa dini, wawe masheikh, wachungaji, mapadri au mtu awaye yote, kushambuliwa, kumwagiwa tindikali wala kuuawa katika matukio yenye hisia na sura za kidini.
Mbowe alisema ni jukumu na wajibu wa serikali kuwahakikishia raia wake usalama wa maisha na mali zao.Alisema chama chake kinaamini katika misingi ya taifa lenye haki, amani, umoja na mshikamano kwa watu wote bila kujali tofauti za kidini na kikabila.
 Mbowe alisema misingi ya watu makabila yote hapa nchini wa imani tofauti za kidini, ya kuishi kwa kuheshimiana na kushirikiana, lazima ilindwe na kuendelezwa kwa kila mtu kutekeleza jukumu lake la kuenzi tunu hiyo iliyoasisiwa na kupiganiwa na waasisi wa taifa.
Katika vipindi tofauti, viongozi wa CCM na serikali yake walikaririwa wakitangaza kuwa Chama cha Wananchi (CUF) na CHADEMA vina misingi ya kidini na kikabila kama moja ya mbinu za propaganda. 
JK aomboleza 
Rais Jakaya Kikwete ameeleza kupokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa kwa Padri Mushi mjini Zanzibar.
Katika taarifa yake kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Kikwete aliwapa pole na rambirambi za dhati ya moyo wake Baba Askofu Shayo wa Jimbo Katoliki la Zanzibar na waumini wote wa Parokia ya Minara Miwili kwa msiba huo mkubwa uliowakuta.
“Napenda kuwahakikishia kuwa tupo pamoja katika kuomboleza kifo cha mpendwa marehemu Padri Mushi na msiba huu ni wa kwetu sote,” alisema.
Rais Kikwete alisema kuwa ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kukusanya nguvu zake zote na maarifa yake yote kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina na wa haraka unafanyika ili kubaini mhusika ama wahusika, na kuwakamata ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.Alisema kuwa anataka ukweli wake ujulikane ili kama kuna jambo lolote zaidi liweze kushughulikiwa na kukata mzizi wa fitina. 

Waziri Nchimbi awasili 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi aliwasili visiwani hapa na kutembelea eneo la tukio alipouawa padre huyo kisha alifanya mazungumzo na waandishi wa habari.Alisena tukio hilo ni la kigaidi, hivyo serikali haitalivumilia kamwe, na kuahidi kulishughulikia ili kuwabaini wahusika.
Nchimbi aliwataka waumini hao kuwa na utulivu kwa kipindi hiki, huku uchunguzi wa kina ukiendelea na kuvitaka vyombo vya ulinzi vya ndani na nje kushughulikia suala hilo.

Je wewe una maoni gani?!

Share this article :

0 comments:

KIKI POLICY


KIKI BLOG POLICY

Blog hii haina lengo la kumdharirisha mtu na pia kutoa taarifa binafsi zenye lengo la kumkwaza mtu,baadhi ya picha na habari katika blog hii hazimilikiwi na KIKI blog bali zinatoka katika vyanzo mbalimbali vya habari. Ikiwa kuna habari au picha yenye kukudharirisha basi usisite kututaharifu mapema hili iondolewe.
KARIBUNI WOTE

BANK WITH DTB 24/7

Blogger Tips and TricksLatest Tips For BloggersBlogger Tricks

WASOMAJI

Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below

Powered By Blogger Widgets

THIS BLOG IS SPONSORED BY:

THIS BLOG IS SPONSORED BY:

KUMBUKUMBU

ZILIZOVUMA

 
----
Support : Copyright © 2015. KIKI NEWS - All Rights Reserved
This blog Designed by and Modified by Joseph Richard