Dar es Salaam. Wamiliki wa vituo vya utangazaji vya televisheni nchini,
wamesema watasitisha kurusha matangazo ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa
kutokana na kushindwa kumudu gharama za uendeshaji.
Hatua
hiyo inatokana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzima mitambo
ya analojia na kuhamia dijitali Desemba 31, mwaka jana kitendo
walichodai kimepunguza mapato yanayotokana na matangazo.
Mwenyekiti
wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), Reginald
Mengi alisema hakuna haja ya kurusha matangazo kwa hasara.
Mengi
alisema kutokana na kuanza kwa mfumo wa dijitali, watangazaji
wamesitisha kutoa matangazo kwa sababu wananchi wengi hawana ving’amuzi.
“Kama
mamlaka itashindwa kurudisha ule mfumo wa analojia kuwa sambamba na
dijitali hadi wananchi watakapokuwa na ving’amuzi, tutazima televisheni
zetu ndani ya mwezi mmoja ujao,” alisema Mengi.
“Ibara ya 18
ya Katiba imekiukwa kutokana na wananchi kunyimwa fursa ya kupata
habari, hivyo hali hii hatutaki iendelee,” alisema Mengi.
Mengi
ambaye pia ni mmiliki wa vituo vya televisheni vya ITV, EATV na Capital
TV, alisema licha ya nchi za Afrika, Tanzania imekuwa ya kwanza kuzima
mitambo ilhali wananchi hawakuwezeshwa kumudu gharama za ving’amuzi.
“Nchi
ambazo zimeendelea kwa kila kitu kama Uingereza, Marekani, Japan na
kwingineko kuzima mitambo ya analojia walitumia zaidi ya miaka minane
kwa nini sisi tumewahi hivi wakati hatujajipanga?” alihoji Mengi.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Sahara Media Group na mmiliki wa Kituo cha Star Tv,
Samwel Nyalla alisema hivi sasa wanaendesha biashara hiyo kwa hasara.
Nyalla alisema hadi mwaka 2015, hali itakuwa mbaya kutokana na kukosa ving’amuzi.
Mkurugenzi
wa Utangazaji wa TCRA, Habby Gunze alisema wao hawakualikwa katika
mkutano huo hivyo hawajui chochote. Gunze alimtaka mwandishi kwenda
ofisini leo.
“Sisi hatujui chochote na kama unataka maelezo
mengine njoo kesho (leo) ofisini kwetu uonane na Mkurugenzi Mkuu
(Profesa John Nkoma), ili tuzungumze kwa ‘fact’ (kwa ushahidi) kipi
kinachoendelea,” alisema Gunze.
Nukuu
“Kama mamlaka itashindwa
kurudisha ule mfumo wa analojia kuwa sambamba na dijitali hadi pale
wananchi watakapokuwa na ving’amuzi tutazima televisheni zetu ndani ya
mwezi mmoja ujao labda TBC ndiyo itakayobaki”.
0 comments:
Post a Comment