Madiwani jijini Dar es Salaam, wameomba kikao cha dharura na Meya wa Jiji, Dk. Didas Masaburi, kutokana na kushitushwa na hatua ya kubadilishwa kwa jina la Benki ya Wananchi wa Dar es Salaam.
Wakizungumza na Tanzania Daima jana, baadhi ya madiwani wa Manispaa ya Ilala na Kinondoni, walieleza kushangazwa na uamuzi uliofikiwa na bodi ya benki hiyo kuamua kuibadili jina benki hiyo na kuwa Dar es Salaam Commercial Bank.
Diwani wa Saranga, Ephraim Kinyafu, alisema wameshangazwa na kubadilishwa kwa jina hilo huku wakishindwa kuwashirikisha viongozi hao ambao ni wawakilishi wa wananchi, hatua inayowafanya wahitaji kikao cha dharura na meya wa jiji.
Naye Diwani wa Segerea, Azurly Mwambaja, alisema benki hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa jiji hilo hivyo kulikuwa na umuhimu wa kujua faida iliyopatikana kabla ya kuhamia katika jina jingine la kibiashara.
Mmoja wa madiwani ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Uchumi, Afya na Elimu hakupenda jina lake litajwe, alisema kuwa ili manispaa kuendelea kuwepo katika bodi wanatakiwa kuchangia sh bilioni 1.2, jambo ambalo linaonekana kushindwa kutekelezwa.
“Ni lazima tufike mahali tuseme hapana, kwani manispaa tatu za jijini ndizo zilizoanzisha benki hiyo kwa mtaji wa sh milioni 500, leo unataka tuchangie fedha ili tuendelee kuwapo katika bodi na kuwa wanahisa, kwani hiyo benki tangu imeanzishwa haijapata faida?” alihoji.
Akizungumzia hilo, Meya wa Jiji, Dk. Masaburi, alikiri kubadilishwa jina kwa benki hiyo na kusema walishirikishwa wanahisa wote kwa kufuata katiba.
“Sijapata taarifa ya madiwani kuhitaji kikao bali ninachofahamu ni kuwa niliwasikia sikia baadhi ya madiwani wakiongea katika kikao cha madiwani cha jiji…kama watahitaji kikao basi nitakiitisha ili tuzungumze,” alisema.