MWANAFUNZI wa 
darasa la sita Shule ya Msingi Kasumulu, Kata ya Ngana, wilayani Kyela, Kaselema 
Mpale (14)  ameuawa kikatili kwa kuchinjwa na kitu chenye ncha kali, kisha 
kunyofolewa baadhi ya viungo vyake sehemu ya mwili. 
Mama mzazi wa 
mwanafunzi huyo, Lucia Kamnyonge alisema tukio hilo lilitokea     Februari 8, 
mwaka huu saa 1:30 usiku, alipotumwa na baba yake kwenda nyumba ya jirani 
kuchukua mpunga ambao ungetumika kwa chakula usiku.
Kamnyonge 
alisema mtoto wake hakupatikanika hadi alipokutwa siku ya pili yake, akiwa 
amechinjwa na kunyofolewa baadhi ya sehemu zake za mwili ambazo ni pua, mdomo, 
jicho, kuondolewa sehemu zake za siri na kuchunwa ngozi ya kichwa karibu na 
utosi na mwili wake kutundikwa juu ya mti. 
Aliendelea kuwa 
baada ya hali hiyo taarifa ilipelekwa ofisi ya serikali ya kijiji, uliitishwa 
mkutano wa wananchi wote na walitawanyika kuanza  kumtafuta mtoto huyo bila ya 
mafanikio.
Baadaye, baba yake alimkuta juu ya mti akiwa ametundikwa kichwa 
chini miguu juu na viungo vyake hivyo vikiwa vimenyofolewa. 
Mwenyekiti wa 
Kitongoji cha Ibungumbati lilipotokea tukio hilo, Adam Mkese alidai tukio hilo 
limewashtua na kwamba, mkutano wa kijiji ulioitishwa kwa dharura wananchi 
walimhusisha baba mzazi wa mtoto huyo na mauaji hayo.
Mkese alidai 
watu wa kijiji hicho walimhusisha kutokana na mazingira tata ya kifo chenyewe na 
maelezo ya kujichanganya aliyoyatoa.
Ofisa mtendaji 
wa kijiji hicho, Naomi  Charles alidai kuna dalili za mzazi huyo kuhusishwa na 
mauaji hayo na kwamba, polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi.
Mwenyekiti wa 
kijiji hicho,  Baruti Mwakasala alidai kuwa hali katika kijiji hicho siyo nzuri 
na kushukuru polisi kwa hatua za haraka walizochukua.
Kamanda wa 
Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na 
kukiri kumshikilia baba mzazi wa mtoto huyo kwa uchunguzi 
zaidi.  
 
 


 
 
 
 
 
 
0 comments:
Post a Comment