BAO pekee lililofungwa na Hamisi Kiiza jana liliiwezesha Simba kuibuka kidedea katika mchezo dhidi ya Coastal Union uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kiiza, raia wa Uganda ambaye alishindwa kuitumikia Simba katika michezo mitatu iliyopita kutokana na kuwa majeruhi, alirejea uwanjani kwa kishindo jana na kuiwezesha timu hiyo kupata ushindi huo mwembamba baada ya kufunga bao hilo dakika ya saba akiunganisha krosi ya Hassan Kessy.
Ni matokeo yaliyopokewa kwa furaha na mashabiki wa timu hiyo, ingawa uchezaji wa timu ulionekana kutowafurahisha mashabiki kiduchu waliojitokeza jana.
Simba iliingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kipigo cha bao 1-0 ilichopata Jumatano iliyopita kutoka kwa Prisons Uwanja wa Sokoine Mbeya, matokeo ambayo yaliwafanya mashabiki wa Simba kuanza kupoteza matumaini ya kufanya vizuri katika mbio za ubingwa wa Ligi kuu Tanzania Bara.
Kutokana na matokeo hayo, Simba sasa imefikisha pointi 18 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya nne ikiwa nyuma ya Mtibwa yenye pointi 19 sawa na Azam, lakini Azam ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa. Yanga bado inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 20 baada ya jana kutoka sare ya mabao 2-2 na Mwadui ya Shinyanga.
Coastal Union itabidi ijilaumu kwa kupoteza mchezo huo kutokana na nafasi kadhaa ilizopata lakini washambuliaji wake walishindwa kuzitumia.
Nafasi hizo zilipotezwa kipindi cha kwanza na Ismail Mohamed, Abasalim Chidiabele na Ibrahim Twaha ‘Messi’ ambao walishikwa na kigugumizi cha miguu kila walipomkaribia kipa wa Simba, Vicent Angban. Nayo Simba pia ilipata nafasi kadhaa za kufunga, lakini pia umaliziaji haukuwa mzuri kila walipokaribia lango la Coastal Union.
Simba: Vincent Angban, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Hassan Isihaka, Justice Majabvi, Said Ndemla, Jonas Mkude, Hamis Kizza/Mussa Mgosi, Mwinyi Kazimoto na Peter Mwalyanzi/Ibrahim Hajib.
Coastal Union; Fikirini Mapara, Hamad Juma, Adeyoum Saleh, Abdallah Mfuko, Tumba Swedi, Yusuph Ssabo, Ibrahim Twaha ‘Messi’/Juma Mahadhi, Mtenje Albano, Abasirim Chidiebere/Ayoub Semtawa , Nassor Kapama na Ismail Mohammed.
Naye Shangwe Thani anaripoti kutoka Shinyanga kuwa Yanga jana ilitoka sare ya bao 2-2 na Mwadui FC kwenye Uwanja wa Kambarage mjini humo.
Kutokana na matokeo hayo Yanga imefikisha pointi 20 ikiendelea kuongoza ligi hiyo, lakini ikiweka rehani nafasi yake ya kuendelea kuongoza ligi hiyo kama Azam yenye pointi 19 itashinda mchezo wake wa leo dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 11 mfungaji akiwa Donald Ngoma, kabla ya Mwadui kusawazisha bao hilo dakika ya 40 mfungaji akiwa Paul Nonga akitumia vyema pasi ya Jerry Tegete.
Mabadiliko yaliyofanywa kipindi cha pili kwa Yanga kuwatoa Malimi Busungu na Andrey Coutinho na kuwaingiza Simon Msuva na Deus Kaseke, huku Mwadui ikiwatoa Jerry Tegete na Jamal Mussa na kuwaingiza Bakari Kigodeko na Athumani Idd, yalionekana kubadili sura ya mchezo kwa timu zote mbili.
Yanga ilipata bao la pili dakika ya 75 mfungaji akiwa Ngoma baada ya kumzidi ujanja beki Joram Mgeveke. Ngoma sasa amefikisha mabao saba nyuma ya Elias Maguri anayeongoza akiwa na mabao nane.
Hata hivyo, wakati mashabiki wakiamini mchezo huo ungemalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi, Kigodeko alibadili sura ya mchezo kwa kuifungia Mwadui bao la kusawazisha dakika ya 88.
Yanga; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Andrey Coutinho, Thabani Kamusoko, Malimi Busungu, Amissi Tambwe na Donald Ngoma.
Mwadui FC; Shaaban kado, Shaaban Hassan, Malika Ndeule, David Luhende, Emmanuel Simwanda, Joram Mgeveke, Anthony Matogolo, Jamal Mnyate, Jabir Aziz, Paul Nonga na Rashid Mandawa. Katika michezo mingine iliyofanyika jana, Toto Africans iliifunga Mgambo Shooting bao 1-0, huku Mtibwa Sugar ikiifunga kagera Sugar bao 1-0.
Nayo Mbeya City ilishindwa kutamba uwanja wake wa nyumbani baada ya kutoka 1-1 na Majimaji, huku pia Ndanda FC nao ikitoka 0-0 na Stand United.
0 comments:
Post a Comment