FAINALI ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka huu itazikutanisha Burkina Faso na Nigeria. Hiyo inafuatia Burkina Faso kuing'oa Ghana kwa mikwaju ya penalti 3-2 jana usiku kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120.
Walipata ushindi huo, baada ya Emmanuel Agyemang Badu kukosa penalti ya tatu kwa kupiga shuti dhaifu.
Lakini Burkinabe watamkosa Jonathan Pitroipa kwenye Fainali Jumapili baada ya kupewa kadi nyekundu dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho.
Ghana ilipata bao la kuongoza dakika ya 13 lililofungwa na Mubarak Wakaso kwa penalti, ambayo ni ya tatu katika mashindano haya, kufuatia beki wa Burkina Faso, Paul Koulibaly kumchezea rafu Christian Atsu.
Burkina Faso ilisawazisha dakika ya 60, wakati Aristides Bance alipofunga kwa shuti la kawaida tu akiwa kwenye eneo la penalti.
Zoezi la mikwaju ya penalti lilianza vibaya kwa Ghana, baada ya Isaac Vorsah kupaisha mkwaju wake na Burkina Faso wakafunga kupitia kwa Bakary Kone, Henri Traore na Bance.
Mechi hiyo ilitanguliwa na mechi kali kati ya Nigeria na Mali iliyokwisha kwa Nigeria kuitandika Mali 4-1 huku Nigeria wakicheza kwenye uwanja amabao walishindwa kufuzu nusu fainali katika mashindano hayo muongo mmoja uliopita.Wakiongozwa na Victor Moses Nigeria waliichachafya Mali na kufanikiwa kufunga bao mbili za haraka haraka kabla ya mchezaji wa Mali kujifunga goli la tatu.Ni Nigeria pia ambao walifanikiwa kuongoza bao la nne kabla Mali kupata bao la kufutia machozi.