Vinara wa Ligi kuu ya vodacom Tanzania bara,Yanga leo wanajitupa uwanjani tena kukipiga na Ruvu Shooting katika uwanja taifa.
Mchezo huo unazikutanisha timu mbili zenye mazingira tofauti kwani Yanga ikitaka kujihakikishia ubingwa mapema wakati Ruvu Shooting ikitaka kuongeza points katika kapu lake.
Yanga itawakabili maafande hao wakiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa mbinde katika raundi ya kwanza wa mabao 3-2.
Ofisa habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alisema timu yake ipo tayari kwa mchezo wa leo na wamekamia kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri kwenye ligi.
Alisema Ruvu Shooting haiidharau Yanga, lakini uwezo wa kusakata kabumbu walionao wachezaji wake unawapa kujiamini na uhakika wa kushinda mchezo huo ambao anaamini utakuwa na ushindani mkubwa kwani Yanga hawatakubali kirahisi kuupoteza.
Mchezo huo ambao utachezeshwa na mwamuzi Jacob Adong wa Mara, viingilio vitakuwa sh 5,000 kwa viti vya kijani na bluu, sh 8,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh 15,000 kwa watakaokaa VIP B na C huku watakaokaa VIP A watalipa sh 20,000.
Mbali na mechi hiyo ya Yanga na Ruvu Shooting, mchezo mwingine wa ligi hiyo leo utakuwa kati ya Toto Africans na Mgambo Shooting katika Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, huku Mtibwa Sugar itakipiga na Coastal Union katika dimba la Jamhuri mjini Morogoro.